Monday, October 26, 2009

TATEDO wawakumbuka watoto walemavu



Peter Edson


TAASISI isiyokuwa ya kiserikali ya TATEDO jana ilikabidhi msaada wa Oveni ya mkaa yenye thamani ya Sh 550,000/= kwenye kituo cha Manzese Day Care kinachojishughulisha na kuwalea watoto wenye ulemavu.

Akikabidhi msaada huo afisa habari wa TaTEDO Editha Mushi alisema taasisi hiyo imeamua kutoa msaada huo kwa wakinamama wanao wahudumia watoto walemavu kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto hao wanapata mahitaji salama na bora.

Alisema thamani ya Oveni inayotumia mkaa ni kiasi cha Sh 550,000 lakini pia kabla ya kuwakabidhi msaada huo waliendesha semina ya siku mbili na kutumia kiasi cha Sh 450,00 , semina elekezi iliyokuwa ikilenga kuwapatia ujuzi wa matumizi sahihi ya jiko hilo

“Tumetumia kiasi cha Sh 1milioni katika shughuli hii ya semina kwa wakinamama 20 pamoja na gharama za kutengeneza jiko hilo lenye uwezo wa kuoka mikate, keki na pamoja na kutumika katika shughuli ya kupika chakula cha aina zote”alisema Mushi.


Naye Mwenyekiti wa kikundi hicho cha wanawake kijulikanacho kwa jina la Manzese Day Care Mery Njoka, mbali na kushukuru kwa msaada huo alitoa wito kwa Serikali kuwa na mpango mkakati na wa muda mrefu wenye lengo la kuondoa fikra potofu iliyojengeka kuwa walemavu ni watu tegemezi

Alisema kituo hicho kina jumla ya walemavu 40 wakiwemo wenye mtindio wa ubongo, wenye vichwa vikubwa, wenye fistula pamoja na waliopinda miguuu.

“Kwa kweli sisi wenyewe hatuwezi kufanya jambo lolote bali tunaamini kuwa kupitia wadau mbalimbali tunaweza ,kufanikisha malengo yetu ya kuwalea watoto hawa walemavu” alisema Njoka.

Alisema pamoja na jitihada nzuri za Serikali zinazoonyesha kila dalili njema za kutaka kuwasaidia watoto walema na wasiojiweza baadhi ya taasisi binafsi zimekosa uaminifu kwa watoto wanaowalea,hivyo alitoa wito kwa taasisi hizo kutekeleza wajibu wao badala ya kuweka mbele maslahi yao kwanza.

Mwisho.

1 comment:

  1. kwa kweli tunawashukuru sana tatedo kwa kuwakumbuka walemavu ni maoni yangu kuwa watu wengine wajitokeze kusaidia walemavu kwani naamini kuwa sisi sote ni walemavu

    ReplyDelete