Thursday, November 12, 2009

16 vyajitosa shindano la kielimu la Zain


Peter Edson
Vyuo vikuu 16 kutoka katika kila pande ya Tanzania jana vilijitokeza katika mchakato wa kuvipata vyuo vikuu vinne vitakavyoshiriki mashindano ya kielimu ya Zain Afrika nchini Uganda mwakani.

Kampuni ya simu za mkononi ya Zain Afrika imekuwa ikiandaa mashindano hayo kila mwaka, mwakani vyuo vikuu vinne kutoka katika nchi za Kenya, Tanzania, Uganda, Malawi, Zambia, Ghana, Sierra Leon na Nigeria ambayo mwaka jana ilitwa ushindi wa shindano hilo vitashiriki kwenye kinyang’anyiro hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana Meneja wa huduma za jamii katika kampuni hiyo Tunu Kavishe alivitaja vyuo vikuu vinavyoshiriki katika mchakato huo kuwa ni Chuo kikuu cha Ardhi, Hubert Kairuki Memorial, Mount Meru, Chuo kikuu cha Muhimbili na Mzumbe.

Vingine ni Chuo kikuu cha Sokoine, St Augustine, St John’s, Teofilo Kisanji, Chuo kikuu Huria, Chuo kikuu cha Tumaini-Moshi, chuo kikuu Arusha, Chuo kikuu Dar es salaam, Chuo kikuu Dodoma, chuo kikuu Zanzibar pamoja na chuo kikuu cha Serikali.
Alisema wanafunzi kutoka katika vyuo hivyo wameandaliwa vya kutosha kwani baada ya Tanzania kushindwa kutamba katika mashindano hayo wamegundua kuwa uelewa mdogo wa wanafunzi nchini ndiyo kikwazo cha kutofanya vizuri.

“Tumejitahidi kuwatafuta wanafunzi ambao tunaamini kuwa watafanya vizuri, tunaendelea na zoezi la kuwashindanisha ili kupata vyuo vikuu vine vitakavyoshiriki mwakani.

“Mara nyingi tumeshindwa kufanya vizuri, kinachotukwamisha ni wanafunzi wetu kutokuwa na uelewa wa kutosha wa mambo yanayojiri duniani, lakini kwa sasa tunaamini mafanikiop yapo,” alisema Kavishe.

Alisema wamepokea jumla ya wanafunzi 64 pamoja na walimu wao 32 kutoka katika vyuo hivyo 16 na kwamba kazi ya kuwashindanisha inaendelea vizuri.

Zain Afrika huandaa mashindano ya kielimu yajulikanayo kwa jina la Zain Africa Challenge kila mwaka na kuvihusisha vyuo vikuu kutoka katika nchi mbalimbali Afrika, washindi wa shindano hilo huzawadiwa dola za Kimarekani 5000 kila mmoja kwa wanafunzi 4, na chuo hupata dola 50,000.